IQNA

Milad un Nabii

Al-Khalil: Wapalestina washerehekea Maulid ya Mtume (SAW) licha ya pingamizi ya Israel

18:03 - September 29, 2023
Habari ID: 3477668
AL-QUDS (IQNA) - Wapalestina waliadhimisha Maulidi yaani kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) huko Al-Khalil na hasa katikak Msikiti Ibrahim huku kukiwa na vikwazo vikali vilivyowekwa na utawala haramu wa Israel ambao unaongoza kampeni ya kupinga Maulidi.

Siku ya Alhamisi, Wapalestina katika mji unaokaliwa wa Ukingo wa Magharibi wa Al-Khalil waliadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) kwa furaha  katika mitaa iliyokuwa imepambwa huku kukiwa na mihadhara kadhaa ya kidini. Hata hivyo, walikabiliwa na vikwazo vizito kutoka kwa wanajeshi wa Israel karibu na Msikiti wa Ibrahim, ambao ulikuwa kitovu cha sherehe hizo za Maulidi.

Idara ya Wakfu ya Kiislamu iliandaa hafla hiyo iliyojumuisha mihadara na qasida za Kiislamu katika msikiti huo unaoaminika kuwa eneo awalimozikwa Manabii  Ibrahim, Ishaq na Yaqub. Msikiti huo unaheshimiwa na Waislamu na Wayahudi na uligawanywa kati ya makundi hayo mawili baada ya walowezi wa Kiyahudi wenye itikadi kali kuwaua Waislamu 29 wa Kipalestina ndani yake mwaka 1994.

Mji mkongwe wa Al-Khalil (Hebron)  pia ulipambwa kwa puto, kamba nyepesi na mabango ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW).

Ghassan Al-Rajbi, mkurugenzi wa Msikiti wa Ibrahim, amesemamsikiti huo umefunguliwa kikamilifu wiki hii kwa ajili ya waumini kusherehekea hafla hiyo. Ameongeza kuwa wanajeshi wa Israel walizidisha hatua zao za kuwakandamiza karibu na msikiti huo ili kuzuia sherehe hizo za Maulidi.

Msikiti wa Ibrahimi na mji wa kale wa Al-Khalil viliongezwa kwenye Orodha ya Turathi ya Dunia ya UNESCO mnamo Julai 2017. Al-Khalil ni mji wenye  Waislamu wa Kipalestina wapatao 160,000 na walowezi 500 wa Israel ambao wanaishi katika maeneo yenye ulinzi mkali.

3485353

captcha