IQNA

Umoja wa Afrika wapongezwa kuitimua Israel kama mwanachama mwangalizi

17:21 - February 07, 2022
Habari ID: 3474902
TEHRAN (IQNA)- Harakati za muqawama wa Palestina za Hamas na Jihad al Islami zimeushukuru Umoja wa Afrika (AU) kwa kuutimua utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye umoja huo na kusema kuwa, hatua hiyo ni pigo kwa zile nchi zinazotangaza uhusiano wa kawaida na utawala huo katili.

Wakuu wa Umoja wa Afrika (AU), jana Jumapili walisimamisha nafasi ya mwanachama mwangalizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika umoja huo na kuunda kamati inayojumuisha wakuu wa nchi saba za Afrika ikiwemo Algeria kushughulikia suala hilo. Mwezi Julai mwaka jana, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat alitangaza kukubaliwa utawala wa Kizayuni kuwa mwanachama mwangalizi wa Umoja wa Afrika bila ya hata kupigiwa kura suala hilo na wala kushirikishwa wajumbe wengine.

Wapalestina wameipokea kwa fuhara hatua hiyo ya kiungwana ya wakuu wa Umoja wa Afrika.Harakati ya Jihad al Islami ya Palestina ikisema kuwa, hatua ya kiungwana ya AU ya kusimamisha uanachama wa utawala wa Kizayuni ambao umepasishwa kwa kauli moja na chombo hicho kikubwa zaidi barani Afrika, ni pigo kwa watu wote ambao wameingia kwenye mkumbo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala katili wa Israel. 

Nayo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS kupitia msemaji wake Hazim Qassim imeushukuru Umoja wa Afrika kwa hatua yake ya kiungwana ya kuutimua utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye umoja huo.

Bunge la Kiarabu

Nalo Bunge la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) limeunga mkono na kusifu hatua ya Umoja wa Afrika ya kukataa utawala wa Kizayuni wa Israel kupatiwa hadhi ya mwanachama mwangalizi katika umoja huo.

Taarifa ya Bunge hilo imeeleza kuwa, uamuzi huo umesahihisha msimamo binafsi wa hapo kabla wa Mkuu wa Kamisheni ya Afrika Moussa Faki Mahamat wa kuupatia utawala huo ghasibu hadhi ya mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika.

Taarfa ya Bunge la Jumuiya ya Nchi za Kiarabu imepongeza msimamo wa kihistoria wa Umoja wa Afrika wa kuunga mkono malengo matukufu ya Palestina na kueleza kwamba, uamuzi wa kukataa Israel kupatiwa hadhi ya mwanachama mwangalizi katika umoja huuo ni ushahdi tosha wa kuunga mkono haki ya taifa la Palestina.

Yemen yaushukuru Umoja wa Afrika

Mjumbe mmoja mwandamizi wa Baraza Kuu la Kisiasa la Yemen amesema kuwa, hatua ya Umoja wa Afrika (AU) ya kuutimua utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye umoja huo ni pigo kubwa kwa wale wanaojipendekeza kwa utawala huo dhalimu.

Muhammad al Houthi amesema kuwa, uamuzi wa Umoja wa Afrika ni pigo kubwa pia kwa zile nchi za Kiarabu ambazo zimejitia kwenye mkumbo wa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni. Vile vile ni pigo kwa nchi zilizoshiriki kwenye kikao hicho cha AU na kuunga mkono kupewa utawala wa Kizayuni hadhi ya mwanachama mwangalizi ndani ya umoja huo. 

Amesema, lakini pigo kubwa zaidi umepata utawala wa Kizayuni ambao imezidi kuuthibitikia kivitendo kuwa jinai zake zinawakasirisha watu wengi ulimwenguni.

3477712

captcha