IQNA

Saudia yaendeleza hujuma za kikatili Yemen

16:38 - May 30, 2015
Habari ID: 3309308
Huku mashambulio makali ya ndege za kivita za Saudi Arabia dhidi ya Yemen yakiwa yanaingia katika mwezi wake wa tatu, maelfu ya raia wa nchi hiyo wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa huku miundombinu ya nchi hiyo ikiharibiwa kabisa.

Ripoti za masharika ya kutetea haki za binadamu na ya utoaji misaada ya kibinadamu zinasema kuwa kufikia sasa watu zaidi ya 4,000 wamepoteza maisha katika mashambulio hayo ya kinyama, 1000 kati yao wakiwa ni wanawake na watoto. Mbali na hayo zaidi ya Wayemen 7000 wamejeruhiwa katika mashambulio hayo wengi wakiwa ni watoto, wanawake na wazee.

Mashirika yaliyotajwa yanasema miundombinu na makazi ya raia pia hayajasalimika na mashambulio hayo ya nchi kavu, bahari na anga, ambapo zaidi ya nyumba 1000 zimeharibiwa. Vituo vya afya vilivyoharibiwa katika mashambulio hayo vinapata 1200. Kuhusiana na suala hilo Shirika la Kimataifa la Misaada ya Kibinadamu Oxfam, limetahadharisha kuhusiana na hali hiyo ya kusikitisha na kuongeza kuwa mashambulio hayo ya kinyama ya Saudia Arabia nchini Yemen yamepelekea zaidi ya watu milioni 16, yaani thuluthi mbili ya watu wa nchi hiyo kukabiliwa na uhaba mkubwa wa maji safi ya kunywa. Linasema hali hiyo ni kengele ya hatari inayoaashiria hatari ya kuzuka janga kubwa la afya nchini Yemen. Oxfam imelaani vikali hatua ya Saudia ya kuendelea kuharibu kwa mpangilio miundombinu ya maji nchini Yemen na kuongeza kuwa jambo hilo limewapelekea Wayemen kunywa maji yasiyo salama kwa afya zao, jambo ambalo limewasababishia maradhi mbalimbali yakiwemo ya malaria na kipindupindu.

Jambo la kusikitisha ni kuwa pamoja na kutolewa kwa takwimu hizo za kutisha lakini jamii ya kimataifa imeamua kukaa kimya na kutochukua hatua yoyote ya dharura kwa lengo la kuzuia umwagikaji wa damu ya Wayemen wasio na hatia. Hali hiyo imekuwa mbaya zaidi kutokana na hatua ya Saudi Arabia ya kuzuia misaada ya kibinadamu iwafikie wahanga wa mashambulio yake huko Yemen. Watawala wa nchi hiyo hata wanawazuia madaktari wasio na mpaka kuwahudumia majeruhi na wahanga wengine wa mashambulio yao ya kichokozi nchini humo. Akizungumzia hali hiyo ya kusikitisha, Daktari Margaret Chan Mkurugenzi Mkuu wa Shrika la Afya Duniani WHO amesema Wayemen wapatao milioni nane na laki sita wanahitajia matibabu ya dharura. Ameashiria uhaba mkubwa wa zana za tiba uliopo huko Yemen na kuongeza kuwa wanawake wengi wajawazito wa nchi hiyo hawana hata suhula za msingi kabisa za kuwawezesha kujifungua salama.../mh

3309101

Kishikizo: yemen jinai saudia Afya
captcha