IQNA

Walowezi wa Kiyahudi kuvunjia heshima Qur'ani Tukufu, wahujumu Msikiti katika Ukingo wa Magharibi

11:43 - June 24, 2023
Habari ID: 3477182
Kamera za usalama zimemnasa mlowezi wa Kiisraeli akiwa na mbwa akirarua kurasa za Qur’ani Tukufu na kuzitupa chini nje ya msikiti mmoja katika kijiji cha Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

 Kitendo hicho cha chuki kilijiri siku ya Jumatano katika kijiji cha Orif, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya utawala wa Israel. Video hiyo pia ilionyesha walowezi wengine waliofunika nyuso zao wakitazama kitendo cha unajisi. Watu hao hao waliojifunika nyuso zao pia walichoma moto shule na kujaribu kuchoma nyumba na msikiti pia, ripoti zinasema. Wakaazi waliviambia vyombo vya habari vya Israel kwamba walowezi hao waliingia katika kijiji hicho kutoka upande wa makazi ya jirani ya Yitzhar. Kisa hicho kinaripotiwa kutokea wakati wa ghasia za walowezi wa Israel katika kijiji cha Ukingo wa Magharibi cha Orif siku ya Jumatano. Hakuna aliyekamatwa kufuatia tukio hili. Hatem al-Bakri, Waziri wa Awqaf na Masuala ya Kidini wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina, amelaani mashambulizi yanayoongezeka ya Israel na walowezi wake dhidi ya misikiti na utakatifu wake. Al-Bakri amesema katika taarifa yake: "Hiki ni kitendo cha kikatili na kisichokubalika ambacho kinaakisi itikadi kali ya mrengo wa kulia ya baraza la mawaziri la Israel, ambayo inayaruhusu magenge hayo ya Kizayuni kufanya jinai za kikatili na za chuki ambazo zinakataliwa na dini zote. Waziri wa Palestina ametaka kusitishwa mashambulizi yote ya Wazayuni dhidi ya misikiti na maeneo matakatifu ya Waislamu huko Palestina, na kuzitaka jumuiya za kimataifa kutekeleza wajibu wao kwani mivutano hiyo inaweza kuzusha vita vya kidini na matokeo yasiyojulikana. Katika taarifa yake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki pia ilikashifu kitendo hicho cha Qur'ani Tukufu, ikitaka wahusika kukamatwa na kuadhibiwa. Walowezi wa Israel walivamia miji kadhaa ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi siku ya Jumanne usiku, wakichoma magari, kuchoma moto mashamba, na kuharibu nyumba, katika matukio yanayowakumbusha mauaji ya kinyama mapema mwaka huu katika kijiji cha Huwwara. Siku ya Jumatano, mamia ya walowezi, wengi wao wakiwa na silaha, walishuka kwenye mji wa Turmusaya, ukilindwa na wanajeshi wa Israel. Walowezi hao waliwashambulia wakaazi wa Palestina, wakaharibu mali zao, na mwanamume wa Kipalestina mwenye umri wa miaka 27 aliuawa kwa kupigwa risasi.

 

3484053

 

Kishikizo: jinai za israel qurani
captcha