IQNA

Hali ya mambo Saudia

Bin Salman wa Saudia ajizuia kushiriki kikao cha viongozi wa nchi za Kiarabu nchini Algeria

19:57 - October 23, 2022
Habari ID: 3475978
TEHRAN (IQNA)- Mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman hatahudhuria mkutano ujao wa kilele wa viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu utakaofanyika nchini Algeria kwa kufuata kile ambacho kimetajwa ni 'ushauri wa madaktari wa kuepuka kusafiri'. Hayo yameelezwa na ofisi ya rais wa Algeria.

Serikali ya Saudi Arabia haijatoa kauli yoyote ya kuthibitisha tamko hilo la Algeria kuhusu hali ya afya ya Bin Salman ambaye amekwea haraka ngazi za madaraka nchini Saudia chini ya utawala wa babake Mfalme Salman mwenye umri wa miaka 86.

Taarifa zilizotolewa kwa Kiarabu na Kifaransa na Idara ya Huduma za Vyombo vya Habari vya Algeria jana Jumamosi zilinukuu taarifa kutoka ofisi ya Rais Abdelmadjid Tebboune kuhusu mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na mrithi wa ufalme wa Saudia.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika mazungumzo hayo ya simu, Bin Salman "aliomba radhi kwamba hatoweza kushiriki katika mkutano wa kilele wa wakuu wa nchi za Kiarabu utakaofanyika Novemba mosi huko Algiers, kutokana na mapendekezo ya madaktari wanaomshauri asisafiri".

Kwa upande wa Saudi Arabia, taarifa ya shirika rasmi la habari la serikali imethibitisha kufanyika mazungumzo hayo kwa njia ya simu kati ya Tebboune na Bin Salman lakini haikuashiria chochote kuhusu ushauri huo wa madaktari. Taarifa hiyo imeeleza kuwa mazungumzo hayo yalihusu "masuala ya uhusiano wa pande mbili kati ya nchi hizo mbili" na uwezekano wa kuwepo ushirikiano wa pamoja.

Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu nchini Algeria utakuwa wa kwanza kwa viongozi wa jumuiya hiyo  kukutana ana kwa ana tangu janga la COVID-19 liliposhika kasi duniani kote.

Arab League, ambayo iliasisiwa mwaka 1945, inawakilisha mataifa 22 kote Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, ingawa kwa sasa uwanachama wa Syria umesimamishwa kufuatia vita vya ndani vilivyozuka nchini humo.

3480967

captcha