IQNA

Jinai za Israel

Mcheza karate wa Kuwait ajizuia kucheza na Muisraeli mjini Baku

17:51 - September 04, 2022
Habari ID: 3475729
TEHRAN (IQNA)-Mpiganaji wa karate wa Kuwait Mohammad al-Otaibi amejiondoa katika mashindano ya 2022 ya Ligi Kuu ya Karate 1 katika mji mkuu wa Jamhuri ya Azerbaijan wa Baku ili kuepuka kukabiliana na mshindani wa utawala haramu wa Israel.

Amechukua hatua yake hiyo kutokana  uungaji mkono wake kwa kadhia ya ukombozi wa ardhi za Palestina zinazokoliniwa na utawala dhalimu wa Israel na pia ni ishara ya kupinga hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo.

Otaibi alipangwa kushiriki katika kitengo cha kumite cha kilo 60 cha kiume cha mashindano ya kimataifa. Hata hivyo, alijiondoa katika mashindano hayo mara tu alipogundua kuwa ameratibiwa kumenyana na mshindani wa utawala wa Israel Ronen Gehtbarg.

Haya yanajiri huku wanariadha kutoka nchi za Kiislamu wakikataa mara kwa mara kushindana dhidi ya wapinzani wa Israel katika mashindano makubwa ya kimataifa kupinga jinai za utawala Israel ambao unaendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.

Hii si mara ya kwanza kwa mwanamichezo wa Kuwait kukataa kucheza na Muisraeli. Mwezi Aprili mchezaji wa  vitara (fencing) kutoka Kuwait, Mohamed Al Fadli alijiondoa katika mashindano ya Ubingwa wa Kimataifa wa Vitara katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ili kujizuia kukutana na Muisraeli.Fadli pia alijiondoa katika mashindano ya kimataifa katika mji mkuu wa Uholanzi, Amsterdam, mnamo Septemba 2019, baada ya droo hiyo kumweka katika kundi linaloshindana na mchezaji wa Israeli.

Aidha mapema mwaka huu, mchezaji maarufu wa mchezo wa tenisi kutoka Kuwait, Muhammad Al Awadi alijiondoa katika Mashindano ya J4 ya tenisi  UAE mjini Dubai ambayo yalifanyika huko Imarati kuanzia Januari 17 hadi 22, ili asikutane na Mzayuni.

Msimamo wake ulipata sifa nyingi kutokana na kuunga mkono mpango wa Palestina, huku wanaharakati wanaoiunga mkono Palestina wakielezea hatua hiyo kama "sehemu ya misimamo ya Kuweit inayounga mkono suala la Palestina" na upinzani wake wa kurejesha uhusiano na Israel.

Kulingana na vyombo vya habari vya Kuwait, Al- Awadi aliibuka mshindi katika mechi zake za kwanza kwenye Mashindano ya Tenisi ya Dubai U-14 na kutinga hatua ya nusu fainali.

Hata hivyo, aliamua kujiondoa katika michuano hiyo mara tu alipoambiwa kuwa anakwenda kukabiliana na mwakilishi kutoka kwa utawala wa Israel.

Mwezi Mei mwaka jana, Bunge la Kuwait lilipitisha kwa kauli moja miswada ambayo inaharamisha mikataba yoyote au kuhalalisha uhusiano na serikali ya Tel Aviv.

Mnamo Agosti 18, 2020, wabunge 37 wa Kuwait waliitaka serikali yao kukataa makubaliano ya kuhalalisha kati ya Israeli na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Hisia za chuki dhidi ya utawala katili wa Israeli zimeongezeka nchini Kuwait. Kura ya maoni iliyofanywa mnamo 2019 na Taasisi ya Washington ya Sera ya Mashariki ya Karibu, ilionyesha kuwa asilimia 85 ya wananchi wa Kuwait wanapinga kuwa na uhusiano na Israeli.

3480337

captcha