IQNA

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon

Silaha za Hizbullah si tatizo kwa Walebanon, watakacho ni maisha bora

8:53 - May 10, 2022
Habari ID: 3475230
TEHRAN (IQNA)- Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrallah ameashiria uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni na kusema tatizo la waliowengi nchini Lebanon si silaha za Hizbullah au Muqawama bali ni hali ya maisha.

Kauli hiyo imekuja huku uchaguzi wa Bunge la Lebanon ukitazamiwa kufanyika Mei 15 na tayari usajili wa wanaowania viti bungeni umeshamalizika na kampeni zinaendelea.

Akizungumza Jumatatu katika mkutano wa kampeni, Sayyid Hassan Nasrallah amesema wale ambao wanataka Hizbullah ipokonywe silaha wamesahau masaibu ambayo watu wa kusini mwa Lebanon wamekumbana nayo mikononi mwa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Nasrallah amesema baadhi ya makundi ya kisiasa nchini Lebanon yanatumia kadhia ya silaha za harakati ya Hizbullah kueneza propaganda dhidi ya harakati hii bila kufahamu kuwa suala ambalo wananachi wanataka kusikia ni kuhusu fedha ambazo zimewekwa katika benki.

Katibu Mkuu wa Hizbullah amesema harakati ya Hizbullah ilihakikisha kuwa mateka waliokuwa wanashikiliwa na utawala wa Israel wanaachiliwa  huru. Aidha amesema Hizbullah inalinda vijiji vya kusini mwa Lebanon vinavyokabiliwa na hatari ya utawala wa Kizayuni wa Israel na kuongeza kuwa tokea 16 Agosti mwaka 2006 vijiji vyote vya kusini vimekuwa na mamlaka kamili kutokana na jitihada za Hizbullah.

Sayyid Hassan Nasrallah amesema wale wanaotaka Hizbullah ipokonywe silaha hawatoi pendekezo mkabala na kwa  hivyo Hizbullah itaendelea kuiilinda Lebanon.

4055844/

captcha