IQNA

Magaidi wa Boko Haram waua watu zaidi ya 25 Nigeria

15:55 - December 20, 2021
Habari ID: 3474700
TEHRAN (IQNA)- Watu wasiopungua 25 wameuawa kufuatia hujuma ya magaidi wa kundi Boko Haram wanaofungamana na kundi la kigaidi la ISIS Tawi la Afrika Magharibi (ISWAP) katika hujuma dhidi ya kijiji kimoja katika mji wa Askira Uba katika jimbo la Borno Kaskazini mwa Nigeria.

Kwa mujibu wa gazeti la Sahara Reporters, magaidi walikuwa wanaendesha magari 10 ambapo waliteketeza pia moto nyumba za maafisa wa serikali akiwemo mkuu wa mji Alhaji Abdullahi Adamu Kilangar.

Hujuma hiyo imekuja masaa machache baada ya Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria kudai kuwa serikali yake imedhoofisha kundi la kigaidi la Boko Haram.

 Kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) Afrika Magharibi, ISWAP, mwezi Juni lilithibitisha katika ujumbe wa sauti kwamba kinara wa kundi la kigaidi la Boko Haram la Nigeria, Abubakar Shekau amejiua na kuelekea jongomeo. Tokea wakati huo ISWAP imeweza kuwachukua wapiganaji wengi wa Boko Haram na hivyo kupelekea kundi hili kugawanyika mara mbili ambapo kuna mrengo uungao mkono ISWAP na kuna mrengo mwingine unaopinga kundi hilo.

Neno Boko Haram kwa ya lugha ya Kihausa, ambayo inatumiwa na aghalabu ya Waislamu wa Nigeria, lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'.

Zaidi ya watu elfu 36 wamepoteza maisha nchini Nigeria tokea kundi la Boko Haram lianzishe uasi mwaka 2009 huku wengine zaidi ya milioni mbili wakilazimika kukimbia makazi yao kutokana na ugaidi wa Boko Haram ambao sasa umeenea katika nchi jirani kama vile Cameroon, Niger na Chad. Halikadhalika ugaidi huo wa Boko Haram umepelekea Waislamu wa kaskazini mwa Nigeria kubakia nyuma kimaendeleo na hivyo kuathiri vibaya mustakabali wao. Serikali ya Nigeria pia inalaumiwa kwa kuzembea katika kukabiliana namagaidi hao huku kukiwa na ripoti kuwa baadhi ya majenerali jeshini na maafisa wa serikali wanaofaidika na ugaidi huo wa Boko Haram.

3477013

captcha