IQNA

Ubalozi wa Israel wafunguliwa Morocco huku kukiwa na malalamiko makali

14:14 - August 13, 2021
Habari ID: 3474185
TEHRAN (IQNA)- Katika safari yake ya kwanza nchini Morocco tangu nchi hiyo ya Kiafrika ianzishe uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa utawala huo ghasibu amefungua rasmi ofisi za ubalozi wa utawala huo mjini Rabat.

Katika safari yake hiyo ya jana, Yair Lapid amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Morocco akiwemo Nasser Bourita Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo na kutiliana saini mikatabaa kadhaa ya ushirikiano katika nyuga za michezo, vijana na utamaduni.

Yair Lapid alifungua ofisi ya kidiplomasia ya utawala haramu wa Israel katika mji mkuu wa Morocco Rabat huku malalamiko ya wananchi wa nchi hiyo ya kupinga serikali yao kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo yakiendelea kushuhudiwa.

Disemba mwaka jana (2020) Morocco na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel zilisaini mapatano ya kuanzisha uhusiano baina yao na kisha Marekani ikatambua rasmi mamlaka ya udhibiti wa Morocco kwa eneo la Sahara Magharibi. 

Morocco ni nchi ya sita ya Kiarabu baada ya Jordan, Misri, Imarati, Bahrain na Sudan  kuanzisha uhusiano kati yake na utawala ghasibu wa Kizayuni.  Kitendo hicho cha Morocco cha kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel ambacho ni sawa na kusaliti malengo ya Palestina kimekabiliwa na radiamali hasi katika Ulimwengu wa Kiislamu na hata ndani ya Morocco kwenyewe.

3990288

captcha