IQNA

Kiongozi Muadhamu: Maombolezo ya Imam Hussein AS huleta rehma ya Mwenyezi Mungu

19:26 - August 11, 2021
Habari ID: 3474179
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema, majilisi za Muharram maombolezo ya Bwana wa mashahidi, Imam Hussein AS zinaletaa rehma na baraka za Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Khamenei ametoa agizo hilo leo alipohutubia taifa kwa njia ya televisheni kuzungumzia hali na mripuko mkubwa wa ugonjwa wa COVID-19 nchini na kuongeza kuwa, nchi na wananchi wanahitaji majilisi hizo zenye baraka, lakini zinapofanyika inapasa miongozo ya kiafya izingatiwe kikamilifu na kwa uzito mkubwa ili kuzuia maambukizi ya COVID-19.   

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amesema kukabiliana na corona ndilo jambo la kwanza na la haraka zaidi la kushughulikiwa nchini.

Aidha amesema kuna ulazima wa kujipanga na kutumia mbinu mpya na madhubuti za kujilinda katika kukabiliana na mabadiliko ya spishi na kasi kubwa ya usambaaji wa kirusi cha corona.

Kiongozi Muadhamu ameongezea kwa kusema: “kupotea roho za watu zaidi ya 500 kwa siku moja na kuziacha familia zao katika msiba na majonzi; na vile vile kuambukizwa maradhi hayo makumi ya maelfu ya watu kwa siku pamoja na matatizo ya kuwapatia tiba watu hao ni jambo linaloumiza mno na kuungulisha moyo wa kila Muislamu na kila mwananchi; kwa hivyo sote tuna majukumu kwa ajili ya kukabiliana na hali hii.”

Ayatullah Khamenei amesema, muhula wa wiki moja uliotolewa na Rais kwa ajili ya kukusanya mapendekezo na maamuzi ya kuchukuliwa kuhusiana na suala hilo ni hatua nzuri; na akaongeza kwamba: suluhisho litakalopendekezwa ndani ya muda huo uliowekwa liwe limetafakariwa kwa umakini, na kwa kila hatua itakayohitajika, uchukuliwe uamuzi madhubuti na kutekelezwa kwa uzito kamili.

Katika hotuba yake hiyo kwa taifa, Kiongozi Muadhamu amesema, machofu makubwa waliyonayo wafanyakazi wa kada ya utabibu na mashinikizo ya kimwili na kiroho waliyonayo yanatia wasiwasi mkubwa na akaongezea kwa kusema: “ninawashukuru kwa udhati wa moyoni madaktari, wauguzi na timu za utabibu, ambazo kwa kweli ziko katika jihadi, ijapokuwa shukrani hasa ni za Mwenyezi Mungu Mshukuriwa na Mjuzi.”

Katika agizo jengine alilotoa kwa viongozi, Ayatullah Khamenei ametiliza mkazo suala la kukidhiwa mahitaji ya chanjo na akasema: bahati nzuri kutengenezwa na kuzalishwa chanjo ndani ya nchi kumefungua njia pia ya kuingizwa chanjo kutoka nje, wakati kabla ya hapo, na licha ya kulipwa gharama za ununuzi wa chanjo, wauzaji wa nje walikuwa wanahalifu makubaliano.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, ikiwa chanjo ni ya kuagizwa kutoka nje au inayotengenezwa nchini, lazima zifanyike juhudi maradufu kuhakikisha chanjo hizo zinakuwepo na kuwapatia wananchi wote.

Amewahutubu pia wananchi kwamba baadhi ya matatizo yanatokana na kutochunga miongozo ya kiafya na akawaasa kwa kusema, wananchi wapendwa wazingatie miiko kikamilifu kwa uzito ule ule wa miezi ya mwanzoni ili wasije wakahatarisha maisha yao na ya wananchi wenzao.

3475479

captcha