Duru za usalama za Palestina pamoja na wakaazi wa viunga vya mji wa Nablus, katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan ambako ndipo lilipo kaburi hilo wamesema, walowezi hao wa Kizayuni waliwasili mahala hapo mapema Alkhamisi wakiwa ndani ya mabasi kadhaa na kuvamia ziara hilo huku wakipewa ulinzi na askari wa utawala haramu wa Israel.
Vikosi vya utawala wa Kizayuni viliweka magari kadhaa ya kijeshi katika barabara inayoelekea kwenye haram ya Nabii Yusuf ili kuzuia kutokea mapigano baina ya Wapalestina na walowezi hao wa Kizayuni.
Muda mfupi baadaye yalizuka makabiliano baina ya askari wa Kizayuni na vijana wa Kipalestina kandokando ya eneo lilipo kaburi la Nabii Yusuf, ambapo askari hao walitumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya vijana wa Kipalestina.
Tukio hilo limejiri siku moja tu baada ya askari wa jeshi la utawala
wa Kizayuni wa Israel na maafisa usalama wa utawala huo ghasibu kuvamia
eneo moja la ardhi huko Ras al-Amud karibu na Baitul Muqaddas mashariki
na kung'oa miche 47 ya mizaituni iliyokuwa imepandwa na Wapalestina kwa
heshima ya kuwaenzi Wapaletsina 47 waliouliwa shahidi na askari wa
Kizayuni katika mji huo mtukufu tangu ilipoanza Intifadha mwezi Oktoba
mwaka jana.