IQNA

Israeli yapendekeza kuipa Saudia makombora kuhujumu Yemen

9:43 - May 24, 2015
Habari ID: 3306968
Utawala haramu wa Israel unapanga kuipatia Saudi Arabia msaada mkubwa wa makombora ili kufanikisha vita vyake dhidi ya watu wa Yemen.

Ripoti zinasema kuwa Israel imeafiki kuipatia Saudi Arabia mfumo wa makombora wa Iron Dome au 'Kuba la Chuma' ili makombora hayo yaimarishe hujuma ya Saudia dhidi ya Yemen. Gazeti la Kiarabu la Rai al-Youm katika toleo lake la Jumamosi limeandika msaada huo uliidhinishwa wiki iliyopita katika mkutano wa siri baina ya maafisa wa Saudi Arabia na Israel katika ubalozi wa Marekani huko Amman, Jordan.

Wiki iliyopita Shirika la Utangazaji la Israel liliarifu kuwa wanadiplomasia wa Israel na baadhi ya nchi za Kiarabu walikutana Jordan katika kikao cha siri.  Katika kile kinachoonekana ni kujaribu kuzuia hasira wa Waislamu duniani, Saudi Arabia imetangaza kukataa msaada huo wa Israel. Kuba la Chuma ni mfumo wa makombora ambao Israel hutumia kukabiliana na wanamapambano wa Palestina katika Ukanda wa Ghaza. Saudi Arabia imetekeleza hujuma nchini Yemen kuanzia Machi 26 ambapo baadhi ya duru zinasema zaidi ya watu 3,000 wakiwemo watoto, wanawake, wazee na raia wasio na hatia wameuawa. Aidha Saudia inayotumia silaha za Marekani imebomoa misikiti, mahospitali, nyumba za raia mbali na kuzuia misaada ya kibinaadamu isiwafikie raia wa Yemen..../mh

3306915

Kishikizo: kombora israel saudia yemen
captcha