IQNA

Sayyid Nasrallah: Hizbullah imejiandaa kwa vita na Israel

9:39 - August 15, 2014
Habari ID: 1439340
Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah amesema kuwa muqawama umejiandaa kikamilifu dhidi ya utawala haramu wa Kizayuni na kwamba katika vita vijavyo na jeshi la utawala huo, hakutakuwa na mstari wowote mwekundu na adui huyo.

Sayyid Hassan Nasrullah amesema kuwa, kile ambacho kimeandaliwa na muqawama dhidi ya adui ni zaidi ya kile ambacho wapiganaji wa Hizbullah wanakitekeleza dhidi ya magaidi huko nchini Syria. Sayyid Hassan ameyasema hayo kupitia mahojiano na gazeti la Lebanon la al-Akhbar kwa mnasaba wa kukumbuka kumalizika vita vya siku 33 kati ya harakati hiyo na jeshi la utawala wa Kizayuni huko Lebanon. Akiashiria kuwa, kuwepo muqawama nchini Syria dhidi ya magaidi hakuna mahusiano yoyote ya kupata maandalizi zaidi dhidi ya jeshi la Israel, amesema kuwa kama vile ambavyo tulilinda mipaka ya maeneo ya kusini mwa Lebanon kwa ajili ya  taifa la Lebanon, ndivyo hivyo tunavyolinda maeneo ya mpakani na Syria kutokana na uwepo wa makundi ya kigaidi. Amesisitiza kuwa, kamwe muqawama hautoi vitisho ambavyo hauwezi kuvitekeleza kwani harakati hiyo imejiandaa kikamilifu kwa ajili ya adui Mzayuni. Akiashiria vita vya utawala wa Kizayuni dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah amesema kuwa, muqawama wa Ghaza unayo haki ya kukabiliana vilivyo na Israel na hatimaye kufikia ushindi. Amesema kuwa vita dhidi ya eneo hilo vimezidisha zaidi mahusiano kati ya harakati mbili za Hizbullah na Hamas dhidi ya adui Mzayuni.

Ikumbukwe kuwa tarehe 14 Agosti 2014, imetimia miaka minane tokea vilipohitimishwa vita vya siku 33 ambavyo vilianzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya ardhi ya Lebanon mwaka 2006. Majeshi ya utawala haramu wa Israel tarehe 13 Julai 2006 yalianza kuishambulia ardhi ya Lebanon, ingawa utawala huo ghasibu ulishindwa kufikia hata lengo moja kwenye mashambulizi hayo. Mapigano kati ya majeshi ya Israel na wanamapambano wa Hizbullah yalihitimishwa baada ya kutolewa azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 14 Agosti 2006. Licha ya kutolewa azimio hilo, utawala huo ghasibu uliendelea kufanya uchokozi wa mara kwa mara dhidi ya ardhi ya Lebanon. Serikali ya Lebanon mara kadhaa imefikisha mashtaka yake kwa Umoja wa Mataifa kutokana na chokochoko zinazofanywa na Wazayuni, lakini umoja huo haujachukua hatua zozote za kivitendo za kukomesha uchokozi na mashambulio ya majeshi ya Israel. Imeripotiwa kuwa, katika vita hivyo vya siku 33 dhidi ya Lebanon, wanajeshi 119 wa jeshi la Israel waliangamizwa na mamia ya wengine walijeruhiwa. Vita hivyo pia vilisababisha raia 1,200 wa Lebanon wengi wao wakiwa wanawake na watoto kuuawa shahidi na maelfu ya wengine kujeruhiwa.

1439289

captcha