IQNA

Ifahamu Qur'ani Tukufu/ 11

Kwanini Qur'ani Tukufu inatajwa kuwa kitabu chenye baraka

8:18 - July 02, 2023
Habari ID: 3477224
TEHRAN (IQNA)- Moja ya sifa zinazotumika kuitaja Qur'ani Tukufu ni ' imebarikiwa’. Sifa hii tukufu inamaanisha nini na kwa nini Mwenyezi Mungu anakielezea Kitabu Hiki Kitakatifu kama kilichobarikiwa?

Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 50 ya Surat Al-Anbiya: “Hii (Qur'ani) tuliyoiteremsha ni makumbusho yaliyo barikiwa, Basi je! Mnayakataa? ?”

Mwenyezi Mungu pia ameelezea mvua na mambo mengine kadhaa kuwa ni heri. Kubarikiwa kunamaanisha kuna baraka nyingi, faida na manufaa ndani yake. Faida hizi zinaweza kutafutwa katika masuala ya kimwili na ya kiroho.

Ili kutathmini neema na baraka za Qur'ani Tukufu na jinsi inavyojenga ufahamu, ingetosha kuzingatia hali za watu wa Bara Arabu kabla ya kuteremshwa Qur'ani Tukufu walipokuwa wakiishi katika umasikini, ujinga, balaa na mifarakano na kuilinganisha na wakati baada ya kuteremshwa Qur'ani Tukufu walipokuwa mfano wa kuigwa kwa wengine. Tunaweza pia kusoma maisha ya watu wengine kabla na baada ya kufahamu Kitabu Kitakatifu.

Imam Ali (AS) kwa nyakati tofauti alielezea hali ya Enzi ya Jahilliyah (wakati wa kabla ya ujio wa Uislamu huko Arabuni), akiwafananisha watu wa Jahiliyah na mtu aliyenaswa katika kimbunga cha kutisha, akilia kila mara kuomba msaada, au mifugo ambao waliokuwa wanaongozwa na wafisadi waliokuwa wakiwapeleka shimoni.

Haya ni baadhi ya mambo waliyoyafanya watu wa Jahiliyah:

  • Walipigana vita kwa visingizio duni, na baadhi vita hivyo vilidumu kwa miaka mingi. Vita hivi viliitwa Ayam al-Arab na baadhi yao vilidumu hadi miaka 40. Watu wa Jahiliyah pia walishambulia ardhi mbalimbali na kuziteka. Hawakujua chochote isipokuwa lugha ya nguvu na panga.
  • Maisha yao yalitawaliwa na ujinga na ushirikina kwa sababu walikuwa mbali na ustaarabu na tamaduni zilizoendelea zaidi. Kwa mfano, ikiwa ng’ombe alikataa kunywa maji, walidai kwamba ni shetani aliyejificha kwenye pembe za ng’ombe-dume, hivyo wangempiga ng’ombe huyo ili kumfanya shetani aondoke.
  • Watu wa Jahiliyah hawakuona thamani yoyote kwa wanawake na waliwaona mabinti kuwa ni aibu. Wengine hata walizika binti zao wakiwa hai.

Mfano mmoja wa baraka za Qur'ani Tukufu ni kuwabadilisha watu kama hao.

Mtukufu Mtume Muhammad (SAW), kwa kutegemea mafundisho ya Qur'ani Tukufu, aliweza kuleta mabadiliko ya ajabu katika jamii na kuiongoza kwenye njia ya mageuzi na uimarishaji wa maadili na fikra. Yafuatayo ni baadhi ya mapendekezo ya kimaadili ya Qur'ani Tukufu kinyume na hali ilivyokuwa katika enzi ya Jahiliyah:

  1. Tahadhari dhidi ya dhulma: “Madhalimu watakuja kujua jinsi mwisho wao utakavyokuwa mbaya. (Aya 227 ya Surat Ash-Shu’ara)
  2. Kusisitiza ikhlasi na ukweli: “Enyi Waumini, mcheni Mwenyezi Mungu, na simameni pamoja na wakweli. (Aya ya 119 ya Surah At-Tawbah)
  3. Kulingania uadilifu: “Kuweni waadilifu mnapohukumu baina ya watu.” (Aya ya 58 ya Surah An-Nisa)

Ni baada tu ya kujifunza kuhusu hali walizoishi watu wa Jahiliyah ndipo tunaweza kufahamu kwa hakika mafanikio makubwa ya Mtukufu Mtume (SAW) na baraka za Quran (katika kuibadilisha jamii hiyo).

captcha