Msemaji wa Baraza la Mahusiano la Waislamu nchini Marekani amesema
chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu nchini Marekani zimekithiri mno tangu
baada ya shambulizi la kigaidi la Paris nchini Ufaransa Novemba mwaka
jana, na hujuma ya makumi ya watu kuuawa kwa kufyatuliwa risasi katika
mji wa San Bernardio jimboni California nchini Marekani Disemba mwaka
huo huo. Hooper amesema chuki hizo ziliongezeka baada ya Donald Trump,
Mgombea wa kiti cha rais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Republican
kutoa pendekezo la kuzuiwa Waislamu kuingia nchini humo eti kwa lengo la
kupambana na ugaidi.
Wakati huo huo Rana Abdulhamid, mtaalamu wa Karate wa daraja ya Ukanda Mweusi ameanzisha kampeni ya kuwapa mafunzo ya kujihami wanawake Waislamu wa Marekani. Mwanamke huyo wa Kiislamu akishirikiana na kundi lake wanatoa mafunzo ya kujihami kwa wanawake Waislamu katika mji wa New York ili waweze kujilinda endapo watashambuliwa na mtu kwa sababu ya chuki za kidini.
Akizungumzia mpango huo, Rana Abdulhamid amesema wanawake Waislamu, sasa wana nyenzo zaidi za kujihami endapo watakabiliwa na vitendo vya kikatili, ikiwemo kukwepa kwa kukimbia au kutumia umahiri wa kupambana ili kujihami.
3483080