IQNA

Tafsiri za Qur'ani Tukufu na Wafasiri / 10

Tafsiri ya Qur'ani Tukufu ya Al-Bayan; matokeo ya mbinu yenye msingi wa Ijtihad

16:51 - December 06, 2022
Habari ID: 3476207
TEHRAN (IQNA) – Kwa kuzingatia mtazamo mpana wa Ayatullah Abolqassem Khoei kuhusu vyanzo vya tafsiri na matumizi yake makubwa ya hoja za kimantiki katika Al-Bayan Fi Tafsir al-Quran, tunaweza kusema mbinu yake katika kuandika tafsiri hii ya Qur’ani inategemea Ijtihad.

Al-Bayan Fi Tafsir al-Quran ni miongoni mwa tafasiri za kisasa wa Qur'ani Tukufu na imekuwa inawavutia wanachuoni tangu ilipoandikwa. Hii ni hasa kwa sababu ya hulka mashuhuri ya kielimu ya Ayatullah Khoei na matumizi yake ya njia yenye msingi wa Ijtihad katika kuandika ufafanuzi.

Ijtihad ni neno la Fiqhi linalorejelea hoja huru ya mtaalamu wa sheria ya Kiislamu, au juhudi kamili ya uwezo wa kiakili wa mwanafaqihi katika kutafuta suluhu la maswala ya Fiqhi.

Al-Bayan Fi Tafsir al-Qur'ani imeandikwa kwa lugha ya Kiarabu na inajumuisha baadhi ya mijadala kuhusu baadhi ya sayansi za Qur'ani kama vile I'jaz (muujiza wa Qur'ani) na Naskh (kufutwa, kanuni ya kufutwa kwa aya ya zamani kwa aya mpya katika Quran).

Kuhusu mwandishi

Seyed Abolqassem Khoei (1899-1992) alikuwa Marjaa Taqlid wa Waislamu wa madhehebu ya Shia na mwandishi wa kitabu chenye juzuu 23 cha Mu’jam Rijal al-Hadith. Mu’jam ni miongoni mwa istilahi zinazotumika katika sayansi za Hadith na inarejelea kitabu ambamo Hadith zimekusanywa kwa kuzingatia maswahaba, miji na makabila.

Ayatullah Mirza Naeini na Ayatullah Mohaqeq Esfehani walikuwa walimu wake wakuu katika Fiqh na Usul. Ayatullah Khoei, katika miaka yake sabini ya kufundisha katika seminari, alifundisha  Fiqhi, Usul na tafsiri ya Qur'ani katika daraja za juu.

Aliwafunza wanazuoni wengi kama vile Seyed Mohammad Baqer Sadr, Mirza Javad Tabrizi, Seyed Ali Sistani, Hossein Vahid Khorasani, Seyed Musa Sadr na Mohammad Is’haq Fayaz.

Nyingi za kazi za Ayatullah Khoei zimekusanywa katika kitabu cha juzuu 50 kiitwacho “Mosu’ah al-Imam al-Khoei.”

Mbinu ya Tafsir

Hadhi ya kielimu ya Ayatullah Khoei na ujuzi wake na Ijtihad katika sayansi ya Kiislamu imemsaidia kutoa maoni na ufumbuzi mpya katika kujadili masuala mbalimbali.

Katika Al-Bayan, anatumia sayansi kama vile filolojia, na huzingatia nukta za kifasihi, kisha hutoa mtazamo wake wa kufasiri au kujadili maoni ya wengine akitegemea uwezo wake wa kielimu.

Miongoni mwa sifa za ufafanuzi huu ni maoni yake ya kina ya kielimu. Kwa kuzingatia malezi yake makubwa ya kielimu, Ayatullah Khoei katika tafsiri ananufaika na elimu yake katika Hadith, Fiqh, theolojia, fasihi, historia, n.k.

Anawakosoa wale wafasiri ambao wamezijadili aya za Qur'ani kwa kipengele kimoja tu, akisisitiza haja ya kuwepo kwa mkabala wa kina wa Qur'ani.

Anasema wafasiri wengi wamezingatia sehemu moja tu ya sayansi ya Qur'ani na kupuuza sehemu nyingine zinazoweza kudhihirisha adhama ya Qur'ani Tukufu. Kwa mfano, anasema, baadhi ya wafasiri wameifasiri Qur'ani Tukufu kwa mtazamo wa kanuni za kifasihi na jukumu la maneno katika sentensi na baadhi kutoka katika nyanja za kifalsafa au kwa mtazamo wa sayansi za kisasa na wote wamefikiria kuwa Qur'ani Tukufu imeteremshwa kwa mtazamo walio nao.

Mtazamo wa mijadala ya kifasihi, kitheolojia, kifasiri na kijamii katika Al-Bayan unaonyesha kwamba Ayatullah Khoei amezifasiri kwa ustadi aya hizo na kujadili maudhui yake kutoka nyanja tofauti. Kwa njia hii, amejaribu kuepuka kuegemea upande mmoja na kutoa tafsiri ya kina ya Aya.

Katika Al-Bayan, amejaribu kwanza kabisa kutoa tafsiri yake mwenyewe ya aya na kisha kutoa uhakiki wa tafsiri za wengine.

Vyanzo vyake katika tafsiri ni Qur'an Tukufu, Hadithi kutoka kwa Ahl-ul-Bayt (AS), mapitio ya msingi wa kiakili na nukta za kifasihi. Kwa kuzingatia mtazamo mpana wa mwandishi kwenye vyanzo vya tafsiri na matumizi yake makubwa ya hoja za kimantiki katika Al-Bayan Fi Tafsir al-Quran, tunaweza kusema njia yake katika kuandika tafsiri hii ya Qur'ani ina msingi wa Ijtihad.

captcha