IQNA

Muhtasairi kuhusu Tafsiri na Wafasiri wa Qur'ani Tukufu/2

Tafsiri kongwe zaidi ya Qur’ani Tukufu ni ile ya Muqatil ibn Sulayman

23:57 - September 28, 2022
Habari ID: 3475851
TEHRAN (IQNA) – Tafsiri kuu ya Qur’ani miongoni mwa kizazi cha tatu cha Waislamu ni ile ya Muqatil ibn Sulayman, mwanazuoni mkubwa na mfasiri wa Qur’ani aliyeishi katika eneo la Khorasan Kubwa.

Kazi yake ndiyo tafsiri kongwe zaidi ya Qur’ani nzima iliyotufikia. Imetajwa na kutumiwa kama marejeo na watafiti na wasomi kwa karne nyingi na kuna nakala nyingi za tafsiri hiyo zinazopatikana leo.

Abolhassan Muqatil ibn Sulayman ibn Bashir Azodi Albalkhi ametajwa kama "kigogo miongoni mwa wafasiri wa Qur’ani". Asili yake ni eneo Balkh (Afghanistan) lakini aliishi Marv (Merv), jiji ambalo sasa liko Turkmenistan.

Inakadiriwa kuwa Muqatil ibn Sulayman alizaliwa mwaka 80 Hijria Qamaria  au 700 Miladia huko Balkh. Kisha akahamia Merv na kuishi huko baada ya kufunga ndoa.  Merv ulikuwa  miongoni mwa miji mikubwa ya Khorasan Kubwa zama hizo na jiji hilo lilikuwa ni makao ya wanazuoni wengi, kama vile Ahmed ibn Hanbal na Sufyan al-Thawri.

Baada ya muda, Muqatil alikwenda Basra na kisha Baghdad, katika Iraq ya leo. Aliishi Baghdad, mji mkubwa ambao ulikuwa kitovu cha elimu na kutembelewa na makundi mbalimbali ya wanazuoni na wanafikra. Huko, alijulikana kwa elimu yake kubwa katika nyanja tofauti na alijulikana kama Sheikh wa Hadithi na Tafsiir.

Chuo cha Kiislamu cha Merv kilijiweka huru kutokana na mapungufu ya elimu ya kieno na hivyo hali hiyo ilimruhusu Muqatil kuandika tafsiri pana isiyojifunga na eneo maalumu. Dibaji ya tafsiri yake inaonyesha kwamba amenufaika na marejeo mbalimbali ya wakazi wa eneo alimokuwa. Mbali na Hadithi na riwaya, Muqatil pia alikuwa ni mwanachuoni wa elimu ya dini na fani nyinginezo.

Sifa hizo pamoja na ukweli kwamba tafsiri yake ilikuwa ya kwanza ya Qur’ani nzima ni nukta ambayo iliifanya kupata umaarufu mara tu baada ya kukamilika.  Umaarufu wake ulikuwa mkubwa kiasi kwamba nakala za kazi hiyo ziliwafikia wanavyuoni wakubwa wa Hadithi katika sehemu mbalimbali za ulimwengu wa Kiislamu na wakatathmini kazi yake.

Katika tafsiri hii, aya zote za Qur’ani zimefasiriwa kwa kufuatana. Amefaidika na Hadithi na hoja na ametumia maneno mafupi na ya muhtasari  na wakati huo huo maneno fasaha. Tafsiri yake inategemea sana ile mbinu ya ‘kutumia Qur’ani kuifasiri Qur’ani’.

Njia ya jumla anayotumia ni kwanza kutambulisha sifa za jumla za Sura, kwa mfano ikiwa ni Makki au Madani na idadi ya aya. Kisha anaifasiri kila aya sehemu kwa sehemu kwa msaada wa aya nyingine. Kisha anafafanua juu ya Sha’an Nuzul (sababu na muktadha wa wahyi).

Kwa kuzingatia umahiri na ujuzi wake, mwandishi huyu  amefaulu vizuri katika kutegemea mbinu ya ‘kutumia Qur’ani kuifasiri Qur’ani’ .

Miongoni mwa vipengele vingine vya tafsiri hii ni kuunda umoja na ushirikiano kati ya aya ambazo maana zake dhahiri zinaonekana kupingana.

Ametaja kwa ufupi na kufanya uhakiki wa mitazamo ya wanazuoni wengine na akaepuka masuala ya mzozo. Faida nyingine ya tafsiri hii ni kwamba ni fupi na inafafanua maudhui kwa muhtasari.

Tafsiri ya Qur’ani Muqatil ibn Sulayman ni muhimu sana kiasi kwamba ingali inatumiwa na wanazuoni baada ya karne kumi na mbili na msomi anahisi kuwa imeandikwa kwa  ajili ya zama za leo ingawa haitumiwi sana na msomaji wa kawaida kwa sababu ya kuwa na maswala ya kitaalamu.

captcha