IQNA

Kiongozi Muadhamu katika mkutano Rais Bashar al Assad wa Syria na ujumbe alioandamana nao

Syria imeibuka mshindi katika vita vya kimataifa na inaheshimika zaidi duniani

21:48 - May 08, 2022
Habari ID: 3475224
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kusimama kidete taifa na serikali ya Syria na kuibuka mshindi katika vita vikubwa vya kimataifa kumeandaa mazingira ya kupata hadhi na kuheshimika zaidi nchi hiyo duniani.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Jumapili mjini Tehran wakati alipoonana na Rais Bashar al Assad wa Syria na ujumbe alioandamana nao hapa Tehran na huku akigusia mafanikio makubwa iliyopata Syria katika medani za kisiasa na kijeshi amesema, leo hii Syria siyo tena ile Syria ya kabla ya vita. Ingawa kabla ya vita miji haikuwa imeharibiwa kama ilivyo hivi sasa lakini heshima na itibari ya Syria sasa hivi ni kubwa zaidi kuliko huko nyuma na nchi zote hivi sasa zinaiangalia Syria kuwa ni dola lenye nguvu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesema, leo hii baadhi ya viongozi wa nchi za eneo hili wanawekwa vikao na kukutana na viongozi wa utawala wa Kizayuni na kunywa kahawa pamoja nao lakini wananchi wa nchi hizo hizo walijitokeza kwa wingi barabarani katika Siku ya Kimataifa ya Quds na kuulaani utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amemkumbuka kwa wema pia Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC na kusema, shahidi huyo mwenye daraja ya juu mbele ya Allah alikuwa na mapenzi makubwa sana kwa Syria na alikuwa akijitolea muhanga kwa maana halisi ya neno kwa ajili ya kulinda usalama wa Syria na matukufu yake kiasi kwamba hatua zake kuhusu Syria hazikutofautiana na hatua zake wakati wa vita vya miaka minane vya kujihami kutakatifu baada ya Iran kuvamiwa na utawala wa wakati huo wa Iraq. 

Aidha amezungumzia jinsi baadhi ya nchi zinavyojifanya ni marafiki wa Syria hivi sasa baada ya kuwa maadui wakubwa wa taifa hilo wakati lilipovamiwa na magaidi kutoka kila upande na kusema, inabidi kuchukua tahadhari na kuwa macho sana na pia kuufanya uzoefu wa huko nyuma kuwa dira iliyo wazi ya siku za usoni.

Kwa upande wake, Rais Bashar al Assad wa Syria amelishukuru sana taifa na serikali ya Iran na pia amemuenzi Shahid Soleimani na kusema, kwa kusimama kwake imara na bila ya kutetereka kwenye misimamo yake katika kipindi cha zaidi ya miongo minne iliyopita kwenye masuala ya eneo hili hususan Palestina, Jamhuri ya Kiislamu imewathibitishia watu wa eneo hili kuwa njia ya Iran ndiyo njia sahahi na ya kimsingi.

4055543

captcha