IQNA

Afrika Kusini, Namibia zapinga Israel kuwa ‘mwangalizi’ Umoja wa Afrika

18:59 - July 30, 2021
Habari ID: 3474140
TEHRAN (IQNA)- Nchi kadhaa za Afrika zinaendelea kupinga hatua ya utawala haramu wa Israel kuidhinishwa kuwa ‘mwanachama mwangalizi’ wa Umoja wa Afrika.

Namibia imelalamikia vikali kitendo cha kuruhusiwa utawala haramu wa Israel kuwa mwanachama mwangalizi au mtazamaji katika vikao vya Umoja wa Afrika (AU).

Katika taarifa leo Ijumaa, Wizara ya Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya Namibia imesema serikali ya nchi hiyo ya Kiafrika imehamakishwa na kutiwa wasi wasi kutokana na hatua ya kutambuliwa utawala haramu wa Israel kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Afrika.

Taarifa hiyo, kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu la Russia imeeleza bayana kuwa, kuruhusiwa Israel kuwa mwanachama mtazamaji wa AU kumeenda sambamba na utawala wa Kizayuni kushadidisha mashinikizo na mbinyo dhidi ya wananchi wa Palestina.

Imesisitiza kuwa, uamuzi huo wa kuudhinisha utawala haramu kuwa mwanachama wa mtazamaji wa AU unakinzana moja kwa moja na malengo na thamani za umoja huo wa kibara.

Aidha taarifa ya Wizara ya Uhusiano na Ushirikiano wa Kimataifa ya Namibia imeashiria kuhusu uungaji mkono wa nchi hiyo ya Kiafrika kwa wananchi madhulumu wa Palestina mkabala wa utawala ghasibu wa Israel. 

Serikali ya Afrika Kusini imepinga kitendo cha kutambuliwa utawala haramu wa Israel kuwa mwanachama mtazamaji katika Umoja wa Afrika (AU.

Serikali ya Afrika Kusini imesema kuwa uamuzi huo si wa kiadilifu na wala hauwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile.

Hatua hiyo ya Afrika Kusini inafuatia uamuzi wa Algeria ambayo pia imekosoa vikali hatua ya Umoja wa Afrika (AU) ya kuupa utawala wa Kizayuni wa Israel kibali cha kuwa mwanachama mtazamaji wa umoja huo.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Algeria sambamba na kulaani vikali uamuzi huo imesema kuwa, hatua hiyo haikubaliki.

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza kuwa, uamuzi huo umechukuliwa pasi na kuweko mashauriano ya hapo kabla baina ya nchi zote wanachama wa Umoja wa Afrika.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria pia imepinga kitendo hicho za Israel kuwa ‘mtazamaji’ katika Umoja wa Afrika na kusema mataifa ya Afrika yataendelea kuunga mkono harakati za ukombozi wa Palestina. Wizara hiyo imesema uamuzi huo ulichukuliwa bila mashauriano na nchi zote wanachama.

Julai 22, utawala haramu wa Israel ulitangaza kuwa umeidhinishwa kuwa mwanachama mtazamaji wa AU baada ya eti jitihada za kidiplomasia za karibu miongo miwili.

3987321

captcha