IQNA

HRW yaituhumu Israel kuwa ilitenda jinai katika vita vya Ghaza

19:46 - July 28, 2021
Habari ID: 3474134
TEHRAN (IQNA)- Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema mashambulio yaliyofanywa na jeshi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel katika vita vya siku 11 dhidi ya Ukanda wa Ghaza yalifikia kiwango cha jinai za kivita.

Human Rights Watch imeeleza hayo katika ripoti ya uchunguzi iliofanya kuhusu mashambulio matatu ya anga yaliyofanywa na Israel , ambayo kwa mujibu wa shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu yalipelekea kuuawa raia 62 wa Palestina.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa, kandokando ya mahali yalikofanywa mashambulio hayo ya anga ya utawala wa Kizayuni huko Ghaza hakukuwepo na vituo vya kijeshi.

Shirika hilo la kutetea haki za binadamu limebainisha katika ripoti yake kwamba, kati ya mashambulio hayo matatu ya anga yaliyofanywa na Israel ni lile la tarehe 16 Mei katika mtaa wa al Wahdah katikati ya Ukanda wa Gaza, ambalo liliteketeza nyumba tatu na kuua jumla ya raia 44, wakiwemo watoto 18 na wanawake 14.

Sehemu nyingine ya ripoti ya Human Rights Watch imeeleza kuwa, shambulio la pili la kombora la ndege za utawala wa Kizayuni lililofanywa tarehe 10 Mei karibu na mji wa Bait Hanun kaskazini ya Ukanda wa Ghaza liliua raia wanane wakiwemo watoto sita.

Kwa mujibu wa ripoti ya HRW, shambulio la tatu ambalo lilichunguzwa na shirika hilo ni la tarehe 15 Mei, ambapo kombora linaloongozwa kutokea mbali lililotengenezwa Marekani lililenga jengo la ghorofa tatu katika kambi ya wakimbizi ya Ash-Shat'i katika Ukanda wa Ghaza na kusababisha vifo vya watu 10 wakiwemo wanawake wawili na watoto wanane.

Wachunguzi wa shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binadamu wanasema, Israel imedai kuwa maafisa wa harakati ya HAMAS walikuwa wamejificha ndani ya jengo hilo, lakini shirika hilo halikupata nyaraka wala ushahidi wowote uliothibitisha kuwepo kituo cha kijeshi katika eneo lililoshambuliwa au karibu yake.

Human Rights Watch imebaini katika uchunguzi wake kwamba, katika mashambulio ya kinyama uliyofanya dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Ghaza, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel ulitumia mabomu yenye shabaha kali aina GBU-31 yaliyotengenezwa Marekani na haukuwa ukitoa tahadhari kwa wakazi wa eneo hilo kabla ya kufanya mashambulio yake.

3475347

Kishikizo: ghaza palestina israel
captcha