IQNA

Wasiwasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria kuhusu afya ya Sheikh Zakzaky

17:19 - October 15, 2019
Habari ID: 3472172
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imetangaza kuwa hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky ni mbaya kutokana na alimu huyo kuendelea kuwekwa kizuizini kwa muda mrefu sasa.

Katika ujumbe iliyotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter, harakati hiyo imeeleza kuwa, baada ya kupita siku 1,401 tangu Sheikh Zakzaky pamoja na mkewe walipokamatwa na kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria, hali ya kiafya ya kiongozi huyo wa kidini inazidi kutia wasiwasi.

Mnamo tarehe 6 Julai mwaka huu, Muhammad Zakzaky, mwana wa kiume wa mwanazuoni huyo mwanamapambano alisema, baba yake amepewa sumu na hali yake kiafya hairidhishi.

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati askari wa jeshi la Nigeria walipovamia na kushambulia Hussainiyah iliyoko katika mji wa Zaria. Katika shambulio hilo, mamia ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Nigeria, wakiwemo wana watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi.

Baada ya jitihada kubwa, maandamano ya kila pembe na mashinikizo mengi ya ndani na kimataifa, mnamo mwezi Agosti, mahakama ya Nigeria iliruhusu Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe wapelekwe India kutibiwa, lakini kutokana na matatizo na vizuizi vilivyowekwa na maafisa wa usalama walioandamana naye, kiongozi huyo wa kidini pamoja na mkewe waliamua kurudi Nigeria baada ya kukaa India kwa muda wa siku mbili tu pasi na kupatiwa matibabu.

Kabla ya hapo, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ilikuwa imefichua kwamba, serikali ya nchi hiyo imekula njama ya kumuua Sheikh Zakzaky kwa kutumia mbinu tofauti ikiwemo ya kumpa sumu.

3849959/

captcha