Akizungumza Jumatatu wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Iraq Salim al-Jabouri mjini Baghdad pambizoni mwa mkutano wa 11 wa Umoja wa Mabunge ya nchi za Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (PIUC), Larijani amebainisha kusikitishwa kwake kwa kuona kuwa, Waislamu hadi sasa wameshindwa kutekeleza majukumu yao kuhusu Wapalestina katika Ukanda wa Ghaza, eneo ambalo limekuwa chini ya mzingiro wa Israel kwa takribani miaka 10 sasa.
Katika mazungumzo hayo Spika wa Bunge la Iran pia amebainisha kuridhishwa kwake na hali ya usalama ilivyo hivi sasa nchini Iraq kufuatia hatua zilizochukuliwa katika kukabiliana na kundi la kigaidi la Daesh au ISIS .
Larijani aidha amesisitiza kuhusu umoja na mshikamano kati ya makundi mbalimbali ya Wairaqi. Kwa upande wake Spika wa Bunge la Iraq ameelezea matumaini yake kuwa, nchi za eneo hili zitaweza kupata utatuzi wa hitilafu zilizopo baina yao.