IQNA

Kiongozi Muadhamu katika mkutano wa Rais wa Uturuki:

Utawala wa Kizayuni unalenga kuunda 'Israel Mpya'

10:37 - October 05, 2017
Habari ID: 3471205
TEHRAN (IQNA)-Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Jumatano alionana na Rais Recep Tayyip Erdogan na ujumbe alioandamana nao hapa mjini Tehran.
Katika kikao hicho, Ayatullah Khamenei alisisitiza kwamba kuna ulazima wa kuongezwa kiwango cha ushirikiano wa nchi mbili kama ambavyo pia ni jambo muhimu sana kuweko maelewano na ushirikiano baina ya Iran na Uturuki katika masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia manufaa ya Marekani na utawala wa Kizayuni katika kura ya maoni iliyofanywa na baadhi ya viongozi wa eneo la Kurdistan la Iraq na kuongeza kuwa, Marekani na madola ya kibeberu hayana mwamana hata kidogo na hivi sasa yanafanya njama za kuanzisha Israel mpya katika eneo hili.

Ayatullah Khamenei amegusia pia matatizo mapya ya ulimwengu wa Kiislamu kuanzia mashariki mwa Asia na Mynamar hadi kaskazini mwa Afrika na kuongeza kuwa, kama Iran na Uturuki zitakuwa na kauli moja katika kukabiliana na matatizo hayo, basi bila ya shaka yoyote makubaliano yao hayo yatafanikiwa na manufaa yake yatakuwa ni kwa nchi zote hizi mbili na kwa ulimwengu mzima wa Kiislamu.

Mazungumzo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, mjini Tehran

Vile vile amesisitizia ulazima wa kuongezwa kiwango cha ushirikiano wa kiuchumi baina ya nchi mbili na kuongeza kuwa, inasikitisha kuona kwamba licha ya kuweko nafasi nyingi sana, lakini kiwango cha ushirikiano wa kiuchumi katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita baina ya nchi hizo mbili hakikuongezeka hata kidogo, hivyo kuna haja ya kufanyika juhudi kubwa zaidi za kunyanyua kiwango cha ushirikiano wa nchi hizi mbili katika uwanja huo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia namna madola ya kibeberu hususan Marekani na utawala wa Kizayuni yanavyofanya njama za kuzishughulisha Iran na Urutuki katika masuala mengine na kuziweka mbali na masuala muhimu ya eneo hili na kuongeza kuwa, madola hayo hasa utawala wa Kizayuni yanafanya njama za kueneza mizozo katika eneo hili.

Kwa upande wake, Rais Recep Tayyid Erdogan wa Uturuki amesema, ukitoa Israel hakuna mtu mwingine yeyote aliyetambua kujitenga eneo la Kurdistan na Iraq na kusisitiza kuwa, nchi zinazopakana na Iraq kamwe haziwezi kukubaliana na jambo hilo.

Vile vile amesema, nchi za Marekani, Ufaransa na utawala wa Kizayuni zinafanya njama za kuzigawa vipande vipande nchi za Mashariki ya Kati. Amesema, madola hayo yanafanya njama hizo hizo pia kuhusu Syria na kwamba msimamo wa pamoja wa Iran na Uturuki katika kuzuia njama hizo ni jambo muhimu sana.

/3649419
captcha